Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ahmad Wa'dhii, mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Baqir al-Ulum (as) na mtaalamu wa nadharia za Sayansi za Kiislamu, aliyasema hayo katika kikao cha “Akili Mnemba na Urithi wa Kiislamu”, kilichofanyika pembezoni mwa Wiki ya Utamaduni ya Iran nchini Urusi, katika mji wa Kazan, Urusi. Akizungumzia tofauti kati ya akili mnemba na kompyuta za kawaida za zamani, alisema: Akili bandia inatofautiana na kompyuta rahisi za zamani; akili mnemba ni mashine ya kidijitali inayojifunza, jambo ambalo kompyuta rahisi za zamani hazikuwa na uwezo huo, mojawapo ya tofauti muhimu pia ni uwezo wake wa kuzalisha maudhui.
Mwanazuoni huyo wa Chuo Kikuu cha Baqir al-Ulum (as) aliongeza: Zamani kompyuta zilikuwa zikiwasilisha urithi uliokuwepo na maudhui ya zamani, lakini akili mnemba yenyewe huzalisha maudhui na kufanya shughuli zinazoelekea katika akili ya asili; ingawa kuna tofauti mkubwa kati ya akili bandia na akili ya asili.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa'dhii, akizungumzia makundi mawili makuu ya akili mnemba, alisema: Tuna akili mnemba ya kutabiri na akili mnemba ya kuzalisha. Katika eneo la uchumi na soko la hisa, akili mnemba ya kutabiri kwa kufuatilia soko, inaweza kukushauri kuhusu hatua unayopaswa kuchukua. Katika eneo la usalama pia inaweza kutabiri mazingira yanayoweza kusababisha kutokea kwa uhalifu katika jamii au kutoa uchambuzi wa haiba za watu.
Mwalimu wa Hawza na Chuo Kikuu aliendelea kusema: Kundi la pili ni akili mnemba ya Generative, yaani akili bandia zalishaji, ambayo katika maeneo kama filamu na muziki inaweza kuzalisha video na muziki, na hata inaweza kubuni usanifu wa jengo, miundo mingi ya aina hii ya akili mnemba huzalisha maandishi, na hata inaweza kuzalisha vitabu.
Mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Baqir al-Ulum (as), akizungumzia uhusiano wa jambo hili na urithi wa Kiislamu, alisisitiza: Kwa kuzingatia kwamba urithi wa Kiislamu, kuanzia Qur’ani, tafsiri, hadithi na vyanzo vyetu, kwa kiasi kikubwa ni maandishi, akili bandia inayozingatia maandishi ndiyo inayozungumziwa sasa katika suala la matumizi yake katika urithi wa Kiislamu.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa'dhii, akifafanua malengo na matumizi manne ya akili mnemba zalishaji katika eneo la urithi wa Kiislamu, alisema: Akili bandia zalishaji inaweza kutumika kwa malengo manne. Kwanza, inaweza kuwa msaidizi wa utafiti, pili, inaweza kuwa na matumizi ya kielimu na kuchukua nafasi ya mwanadamu katika kufundisha.
Aliongeza: Mwaka uliopita katika Chuo Kikuu cha Harvard, wanafunzi waligawanywa katika makundi mawili; baadhi yao walifundishwa kwa kutumia akili mnemba, na wengine walifundishwa na mwalimu. Wale waliofundishwa kwa kutumia akili mnemba walipata viwango bora zaidi kuliko kundi lile la wanafunzi waliofundishwa na mwalimu.
Mwalimu huyo wa Hawza na Chuo Kikuu alitaja matumizi ya tatu kuwa ni matumizi ya watu wa kawaida ya akili mnemba kwa ajili ya kupata taarifa kuhusu Uislamu na Sayansi za Kiislamu, akasema: Watu wa kawaida wanaweza kuielekea akili bandia kwa ajili ya kupata taarifa kuhusu Uislamu na Sayansi za Kiislamu.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa'dhii aliendelea kusema: Lengo la nne, ambalo lina umuhimu zaidi, ni kujiuliza iwapo akili mnemba inaweza kupata nafasi ya mamlaka ya kiakili badala ya wanazuoni wa dini. Muislamu hujifunza itikadi zake za kidini kwa kurejea kwa wanazuoni wa dini, na mwanazuoni huyo huwa marejeo yake ya kiakili, Muislam kwa kumwamini mwanazuoni huyo, hupata itikadi zake.
Vilevile katika eneo la Sheria, Muislamu hutekeleza namna ya kuswali, kuhiji na ibada nyingine kwa kutegemea fatwa ya faqihi na mwanazuoni wa dini; kwa hiyo swali linalojitokeza ni kwamba: Je, badala ya kumwamini mwanazuoni wa dini, tunaweza kuiamini akili mnemba?
Akiwa anaeleza kwamba kwa mtazamo wake, mbadala huo hauwezekani, alisema: Kwa mtazamo wangu, jambo hili haliwezi kutokea. Akili mnemba inaweza kutumika kwa kiwango fulani katika malengo matatu ya kwanza. Uwezekano wa kosa au makosa upo katika kila chanzo, lakini katika masuala ya imani na itikadi zetu za kidini, hatuwezi kupuuza makosa yanayotokea.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa'dhii, akizungumzia namna akili bandia inavyofanya kazi, alisema: Algoriti ambazo akili mnemba inazo hazijawekwa kwa namna ambayo akili hiyo inalazimika kutumia maudhui sahihi na yanayolingana na uhalisia. Akili bandia zalishaji ya maandishi hufanya kazi kwa kuweka taarifa pamoja kipande baada ya kipande na kutabiri kile ambacho kinaweza kuwa katika aya inayofuata.
Aliongeza: Algoriti za chatiboti hizi zimejengwa kwa msingi wa kutoa maandishi yanayoaminika na yanayokubalika, si lazima maandishi yaliyo sahihi na yanayolingana na ukweli. Mara nyingi imetokea kwamba ChatGPT imebuni taarifa au imetaja chanzo ambacho hakikuwepo kabisa, kwa sasa hatuna chatiboti ambayo inapobaini kwamba taarifa fulani si sahihi, hukataa kuitoa; vilevile inaweza kutaja chanzo ambacho hakina uwepo wa kweli.
Mwalimu huyo wa Hawza na Chuo Kikuu, akizungumzia wingi mkubwa wa data uliopo mikononi mwa chatiboti, alisema: Kiasi kikubwa cha data kilicho mikononi mwa ChatGPT kina maudhui mengi zaidi kuliko taarifa zisizo sahihi, na mfumo huu hurejea katika kila kitu kinachopatikana kwenye intaneti. Hakuna mtu anayeweza kusema kwamba kiwango cha maudhui batili katika “Big Data” hii ni kikubwa kuliko maudhui sahihi; bali kinyume chake, kiwango cha maudhui sahihi ni kikubwa zaidi kuliko taarifa zisizo sahihi.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa'dhii alihitimisha kwa kusema: Kwa sababu hiyo, akili mnemba ni nzuri na yenye manufaa kwa malengo matatu ya kwanza niliyoyataja, na inaweza kuwa na ufanisi mkubwa kabisa; lakini kwa lengo la nne, yaani kupata imani na itikadi zetu kutokana na maudhui ambayo wakati mwingine huwa yamebuniwa, haiwezi kuaminika. Akili mnemba, kutokana na makosa hayo, kamwe haiwezi kuchukua nafasi ya mwanazuoni wa dini katika kujenga imani na kuwa msingi wa utekelezaji wa Sheria.
Maoni yako